Sunday, June 17, 2012

KUGOMBEA MADARAKA AFRIKA NI JADI YETU?

Hadi sasa Afrika imegawanyika katika mafungu mawili ya kusini na magharibi huku kaskazini ikiachwa kama ilivyo labda kwa sababu haitaki kuhusishwa au inashangaa nini kinachoendelea.

Nasema kaskazini ni kama inashangaa kinachoendelea kwa sababu moja kubwa kwamba haina uhakika kwamba nayo ni moja kati ya kanda zinazounda Umoja wa Afrika licha ya kuwa na viti katika umoja huo mkongwe Duniani.

Mafungu mawili yamekuja au yametokea si kwa sababu mpya ama ambazo waafrika hawazijui au ulimwengu kwa ujumla hauzijui,sababu zipo hadharani sana hata kwa vijana wanaokuwa hapa Afrika kwani ni wimbo kama zilivyonyimbo nyingine UROHO WA MADARAKA.

Tume ya Umoja wa Afrika ambacho ni chombo kimojawapo kati ya vyombo muhimu vya Umoja huo,kutokana na kazi zake nyingi ikiwemo ya kutatua migogoro,kusisitiza na kusimamia amani kwa mataifa wanachama,kiko kwenye mgogoro wa kiuongozi uliosababisha mpasuko wa pande mbili nilizotaja awali.

Chanzo cha mpasuko ni uchaguzi uliofanyika kwenye makao makuu ya AU Addis Ababa nchini Ethiopia kwenye mkutano uliopita ambapo pamoja na kuwa na wagombea wengine lakini Mwenyekiti wa sasa Jean Ping aliyekuwa anamaliza muda wake na mgombea toka kusini mwa Afrika hususan Afrika Kusini mtalaka wa Rais Jacob Zuma,Bibi Nkhosazana Dlamin Zuma walichuana vikali lakini hakuna aliyepata kura za kutosha kuchukua kiti hicho.

Mkutano uliamua uchaguzi urejewe kwenye mkutano ujao wa AU ambao umerejeshwa Addis Ababa kutoka Malawi baada ya taifa hilo kudai haliko tayari kumwona Rais wa Sudan Omar Al bashir akiwa huru katika ardhi yake mwanachama wa mahakama ya  ICC The Hague ambaye kwa sasa anabembeleza hisani ya mataifa ya magharibi ili arejeshewe mikopo baada ya kukumbwa na ukata mkubwa ambao unamfanya Rais Joyce Banda kujipanga kuuza ndege ya Rais aliyonunua marehemu Rais Bingu wa Mutharika kwa madai kwamba,anajali wananchi.

Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC iliwakutanisha mawaziri wa mambo ya nje wanachama wake hivi karibuni moja kati ya agenda kuu ilikuwa ni kujipanga na kuweka mkakati kamambe wa kuhakikisha Zuma anashinda kwenye uchaguzi ujao,na inasemekana mataifa ya magharibi nayo yalikwisha kutana kuweka mkakati wa kuhakikisha Ping anashinda kwa kishindo ili arejee kwa awamu nyingine katika kiti cha uenyekiti wa Tume ya Afrika.

Mikutano ya kuweka mambo sawa imekuwa ikifanyika na hata mwingine ulisababisha wajumbe wakutwe na dhahama ya kutorejea makwao kwa wakati baada ya mapinduzi ya kijeshi .

Najiuliza nini kinachoifanya AU isikae kutafakari maendeleo ya waafrika zaidi ya kutatua migogoro ya kisiasa kila siku kama si uroho wa madaraka?

Mataifa wanachama wanajifunza nini katika mgogoro na mgawanyiko uliopo sasa katika chombo hicho?

Je katika hali hii migogoro itaisha Afrika?

Je katika hali hii,ipo siku ndoto ya Afrika kuwa na Serikali moja itatimia kama walivyotabiri akina Kwame Nkhuruma,Julius Nyerere,Jomo Kenyatta,Muamar Khadafi n.k

Je kama hali iko hivyo katika chombo kikubwa kama hicho,itakuwaje kwa vyombo vingine vya kikanda kama ECOWAS,SADC,EAC,COMESSA n.k.

KARIBUNI.

 

No comments:

Post a Comment