YALIYOMO

Wednesday, June 5, 2013

MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2013 ZAINGIA ARUSHA.




Mkuu wa mkoa wa Arusha Bwana Magesa Stanslaus Mulongo ameelezea takwimu mbalimbali za mkoa wa Arusha katika mapambano dhidi ya Ukimwi,dawa za kulevya na rushwa ambavyo ndivyo vinavyosisitizwa na ujumbe wa mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu 2013.

Bwana Mulongo ametoa takwimu hizo wakati akipokea mwenge huo kutoka mkoa wa Manyara katika kata ya kansai iliyopo kwenye mpaka wa mikoa hiyo miwili ambapo mbio za mwenge sasa ziko rasmi katika mkoa wa arusha ambapo miradi mbalimbali itazinduliwa.

Mkuu wa mkoa amemweleza Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Bwana Juma Ali Simai kwamba;wananchi wa mkoa wake wameendelea kujitokeza kupima ukimwi kwa hiyari mwaka hadi mwaka na kwamba,watu 122,442 wamepima ukimwi tangu julai mwaka jana hadi sasa.

Amesema kati ya waliopima wanawake walikuwa 70,313 na wanaume ni 52,129 ambapo jumla ya watu 1,834 walikuwa na virusi wanawake wakiwa 989 na wanaume 845 na kwamba kwa takwimu hizo kiwango cha maambukizi mapya kimepungua kutoka asilimia 1.6 cha juni mwaka jana hadi asilimia 1.49 hivi sasa.

Kuhusu biashara na matumizi ya dawa za kulevya Bwana Mulongo amesema,biashara imekuwa kubwa na watumiaji wameongezeka ambapo hadi sasa jeshi la polisi limeweza kukamata kila 77,581 za bangi,22,172 za mirungi na gramu 790 za kokein.

Aidha tangu julai mwaka jana hadi sasa jumla ya watuhumiwa 374 walihusika na makosa hayo na jumla ya kesi 140 zinazo husiana na dawa za kulevya ziko mahakamani.

Kuhusu takwimu za rushwa,mkuu wa mkoa amesema;mkoa umepokea taarifa 89 zinazohusiana na vitendo hivyo kuanzia mwaka jana hadi sasa na kesi kumi ziko mahakamani.

Mwenge wa uhuru ukiwa mkoani Arusha utafanya kazi ya kuweka mawe ya msingi,kuzindua na kufungua jumla ya miradi 54 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.9.


No comments:

Post a Comment